Stephano Simbeye, Mwananchi
VWAWA: Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbozi mkoani
Songwe kimemuondolea udhamini Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Erick
Ambakisye kwa madai ya kushindwa kuisimamia halmashauri, na kusababisha upotevu
wa fedha za umma na upatikanaji wa hati zenye mashaka kwa miaka minne mfululizo.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Katibu wa chama wilayani hapa
George Silindu kuwa kamati ya siasa ya chama hicho iliyokutana April mosi mwaka
huu kiliazimia kuondoa dhamana yake kufuatia tuhuma mbalimbali zinazomkabili
ambazo zimesababisha chama hicho kukosa imani kwa wananchi.
Alizitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni upotevu wa Sh.
410milioni ambazo chama hakijui mstakabali wake kwa muda mrefu, kupatikana na
kwa hati zenye mashaka kufuatia ukaguzi unaofanywa na Mdhibiti na mkaguzi wa
hesabu za serikali kwa miaka minne mfululizo na kushindwa kusimamia maamuzi ya
kuweka makao makuu ya kata ya wasa kwa kutofautiana na chama.
Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Mbozi Aloyce Mdalavuma
alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuona kiongozi huyo hakidhi matakwa ya
chama, ambapo makosa yake yamesababisha malalamiko mengi toka kwa wananchi
kufuatia mwenendo mbovu wa halmashauri ya Mbozi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya Mbozi Erick
Ambakisye akizungumzia suala hilo alisema hajapata rasmi barua ingawa amekuwa
akisikia yakizungumzwa mtaani, hata hivyo alisema kinachoendelea kinatokana na
mambo ya kisiasa na vita dhidi ya nafasi ya uenyekiti na uchaguzi mkuu wa 2020.
Alisema vita hiyo ilianza muda mrefu ambapo yamekuwepo
majaribio mara sita ya kutaka kumuondoa kwa njia ya kushawishi madiwani kupiga
kura ya kutokuwa na imani naye, majaribio ambayo hayakuzaa matunda.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Lusajo
Mwalukasa amekiri kupokea barua kutoka kwenye chma cha mapinduzi ikimuagiza
kumjulisha mwenyekiti huyo kuwa ameondolewa udhamini, hata hivyo alisema
taratibu za kumuondoa mwenyekiti zimekiukwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazoendesha
halmashauri vifungu vya 82 (1) (a hadi E) ambavyo vinaenda sambamba na tangazo
la serikali namba 262 la 1998.
Aliongeza kuwa taratibu za kumuondoa mwenyekiti wa
halmashauri ambaye ni kiongozi wa baraza la madiwani wa vyama vyote ambao ndiyo
waliomchagua zinataka ipatikane orodha 2/3 ya wajumbe wa baraza la madiwani na kasha
kuweka sababu za kutaka kumuondoa, ambapo mkurugenzi atamuandikia mwenyekiti
ambaye atahitajika kuzijibu kwa muda wa siku tano kwa maandishi ikiwa ni
utetezi wake.
Mwisho
No comments:
Post a Comment