Stephano Simbeye, Mbozi
Jeshi la Polisi wilayani Mbozi mkoani Songwe, jana
limeteketeza pombe za viroba zilizokamatwa kwenye operasheni iliyofanywa hivi
karibuni zenye thamani ya zaidi ya Sh. 2.5 milioni, baada ya washitakiwa
waliokamatwa wakiviuza, kesi zao kutolewa hukumu na mahakama ya mwanzo Vwawa
mjini.
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo Mkuu wa operesheni wa
jeshi hilo Mkaguzi wa Polisi Simon Mwavea amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya
watuhumiwa kufikishwa mahakamani na kutolewa hukumu ambapo wahusika wamepewa adhabu mbalimbali ikiwemo kifungo na
wengine kulipa faini.
Alisema operasheni ya kukamata viroba katika mji wa Vwawa imesaidia
kupunguza matukio ya uharifu baada ya vijana waliokuwa wanalewa asubuhi, kuacha
kufanya hivyo na kuanza kufanyakazi ambapo wengi wamejiajiri kwenye bodaboda,
wengine katika vibarua mbalimbali ikiwemo kazi za shambani.
Mwavea ameonya wale wote ambao bado wanaendelea kuuza viroba
kwa kuvipa majina tofauti kuwa jeshi hilo linaendelea na operesheni na
watakaokutwa navyo hatua kari zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kunyang’anywa na
kufikishwa mahakamani, pia amewataka viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa
kuacha kuwalinda wauza viroba.
Mmoja wa wananchi aliyeshuhudia zoezi la kuteketeza viroba
hivyo Manuel Kaminyoge amesema kutokana na urahisi wa upatikanaji vinywaji
hivyo vilisababisha ulevi ambao ulikuwa chanzo cha matukio ya uharifu na pia unarudisha
nyuma uchumi wa vijana na taifa kwa ujumla.
aidha mara baada ya viroba kupigwa marufuku na serikali wauzaji wamebuni mbinu mpya ya kuuza kwa kuviita majina mapya ya Sub ufa, maziwa fresh, biscuti na mengine mengi
Mwisho
No comments:
Post a Comment