Social Icons

Saturday, 22 April 2017

Sakata la Kuondolewa Udhamini Mwenyekiti wa Halmashauri laendelea kutesa



 Stephano Simbeye, Mbozi


SAKATA la kuondolewa dhamana, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbozi mkoani Songwe  madiwani 20 kati ya 39 wa halmashauri hiyo,wamesusia vikao vilivyofanyika April 20 na 21 mwaka huu na kutoka nje ya ukumbi kwa madai ya kupinga mwenyekiti anayeongoza vikao hivyo Erick Ambakisye uenyekiti wake uliondolewa dhamana na kamati ya siasa ya CCM kwa kushindwa kuisimamia halmashauri na kusababisha upotevu wa Sh. 410milioni na kupatikana kwa hati za mashaka miaka minne mfululizo ndani ya uongozi wake.

Ambakisye aliondolewa udhamini na Chama Cha Mapinduzi (CCM)  April mosi mwaka huu, hivyo kukosa sifa za kuwa mwenyekiti na kupelekea madiwani 15 wa UKAWA na wa 5 wa CCM kutoka nje ya ukumbi wakidai mwenyekiti huyo hana sifa ya uenyekiti huku madiwani 19 wakiendelea na kikao cha kupitisha taarifa za kata na baraza kamili cha April 21 mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kutoka nje ya ukumbi,mwenyekiti wa kambi ya upinzani Maarifa Mwashitete,alisema mapema mwezi April mwaka huu chama hicho kupitia Katibu wake Kaimu Katibu George Silindu kilitoa tamko mbele ya waandishi wa habari kuhusiana na hatua iliyochukuliwa na Kamati ya Siasa wilayani hapa na kuwasilisha barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri kwa ajili ya hatua zaidi za kumsimamisha uongozi na kumtaja makamu Mwenyekiti wa halmashauri Alan Mgula kukaimu nafasi hiyo.

Alisema kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuwa diwani anapatikana kupitia chama cha Siasa, hivyo kama chama chake kikiondoa dhmana anakosa sifa ya kuwa diwani kama ilivyofanyika kwa kamati ya siasa ya CCM kuondoa dhamana kwa mwenyekiti huyo.

Alisema chanzo cha Mwenyekiti huyo kuondolewa ni kushindwa kuwajibika na kuisababishia halmashauri hiyo kupata hati zenye mashaka kwa miaka minne mfurulizo na kibaya zaidi alisema mwenyekiti huyo,amesababisha ubadhirifu wa fedha million 410 pamoja na milioni 70 za ujenzi wa ghala la Mlowo.

Alisema serikali ilitoa milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa ghala hilo lakini ujenzi haujafanyika na fedha hazionekani na kwamba mbali na hilo kuna ubadhirifu mwingi katika ujenzi wa miradi mingine hali inayopelekea mwenyekiti huo kushindwa kusimamia majukumu yake ya kazi hivyo alisema hawapo tayari kufanya nae kazi.

Naye Katibu wa madiwani wa CCM katika halmashauri hiyo,George Msyani alikiri kuwepo na tuhuma hizo na kusema kuwa yeye ni mjumbe wa kamati ya Siasa na diwani kata ya Nanyala alikuwepo katika harakati za kumvua udhamini mwenyekiti huyo kutokana na kuwepo kwa tuhuma lukuki za ubadhirifu.

Alisema baada ya kupeleka muhtasari wa kuondoa udhamini kwa mwenyekiti huyo,kwa mkurugenzi,mkurugenzi aliwapa kanuni za taratibu za kumvua uenyekiti ambayo inakinzana na kanuni iliyotumika kwenye kamati ya siasa hivyo wanatakiwa kujipanga upya.

Aliongeza kuwa licha ya kuwepo kwa tuhuma za ubadhirifu katika halmashauri hiyo,lakini kumekuwepo kwa vita ya kisiasa ambayo baadhi ya vigogo wanadhani mwenyekiti huyo anajipanga kugombea Ubunge 2020.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni diwani kata ya Bara Aloyce Mdalavuma alisema kamati ya siasa imeondoa udhamini kwa mwenyekiti huyo lakini walipopeleka barua kwa Mkurugenzi ilionekana kanuni ya halmashauri inakinzana na kanuni waliyoitumia.
Alisema suala hilo linasubiri uamuzi mwingine wa chama na kuwa iwapo maamuzi mengine yatatolewa wananchi watajulishwa lakini kwa wakati huu waendelee kusubiri

 ‘’Ni kweli wananchi wamekosa imani na utendaji wetu katika halmashauri hii,kupata hati nne mbaya inatukosesha amani kwa wananchi” alisema Mdalavuma.

Kwa Upande wake mwenyekiti Erick Ambakisye,alisema njia iliyotumika kumuondolea udhamini haikufuata taratibu  kwani kufuatia sakata hilo hakuna sehemu alipoitwa kuhojiwa na ngazi yeyote ya chama na kuwa kutokana na mapungufu hayo Mwenyekiti wa chama anapaswa aitishe mkutano na waandishi wa habari ili kukanusha sintofahamu iliyojitokeza na kuwa hayo ndiyo makubaliano mapya yaliyofikiwa.
Mwisho



No comments:

Post a Comment