Social Icons

Saturday, 15 April 2017

Ugomvi wa Kugombea Makao makuu ya Kata Wasababisha vijiji kutoshirikiana



Stephano Simbeye, MBOZI

Wakazi wa Vijiji  vya Wasa na Malolo katika kata ya Wasa wilayani Mbozi mkoani Songwe wamevunja ushirikiano  wa kijamii na wenzao wa vijiji  vya Isalalo na Izyaniche kutokana na ugomvi wa kugombea makao makuu ya kata hiyo, na kumzuia ofisa mtendaji kata na kijiji cha Wasa, mpaka serikali itakaporejesha ofisi za kata katika eneo zilipokuwepo awali.

Sakata hilo ambalo limedumu takribani miaka miwili sasa linadaiwa ni kufuatia uamuzi wa diwani kata hiyo kuamua kuhamisha ofisi za kata hiyo toka kijiji cha Wasa na kuzihamishia kijiji cha Isalalo kwa kigezo cha kuwa ni katikati ya vijiji vyote vinne vinavyounda kata hiyo jambo ambalo liliibua mgogoro baada ya wananchi wa vijiji viwili vya Wasa na Malolo kupinga wakidai kuwa vijiji vyao vina wakazi wengi.

Joseph Sinkonde mkazi wa kijiji cha Wasa alisema  wameamua kumzuia mtendaji wa kijiji kufanyakazi kijijini hapo hadi pale ambapo serikali itakaporejesha ofisi za kata katika kijiji cha Wasa zilipokuwa tangu kuanzishwa mwaka 2015.

“ kutokana na kitendo hicho cha kuhamisha makao makuu ya kata toka Wasa kwenda Isalalo hatuko tayari kushirikiana na watendaji wala serikali tutabaki na shida zetu mpaka kitakapoeleweka” alisema Sinkonde.

Mawazo  Andondile alisema suala la mgogoro wa kugombea makao makuu ya kata limeathiri pia mahusiano ya kijamii, watu hawauziani wala kununuliana alitoa mfano kuwa  kila tarehe 8 ya mwezi katika kijiji cha Isalalo kunafanyika gurio, lakini watu wa Wasa na Malolo hawashiriki, na hata katika shughuli za misiba wameacha kushirikiana wakihofia kudhuriana kutokana na mgogoro huo.

Alisema mgogoro huo umeenda mbali zaidi baada ya wanafunzi 84 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Isalalo mwaka huu wamehamishwa shule hiyo  na wazazi wao, na kuwahamishia shule jirani ya Msia  kutokana na hofu ya mzozo huu kwa  usalama wao.

Mmoja wa wazazi wa wanafunzi waliohamishwa shule hiyo Wiliadi Mnkondya alisema uamuzi wa kumhamisha mwanaye ni kutokana na kukosekana kwa amani kufuatia  hofu ya usalama wa mtoto wake na kudai kuwa hata hivyo shule ya Msia iko karibu ukilinganisha na Isalalo.

Mkazi wa kijiji cha Isalalo Joseph Damiani alisema uamuzi wa kuweka makao makuu ya kata kijiji cha Isalalo ulikuwa sahihi ili kuwasogezea huduma  wakazi wa vijiji viwili kati ya vinne vinavyounda kata hiyo ambavyo viko  mbali na huduma za kiserikali hali iliyosababisha kujiona kama wametengwa na serikali yao.

Alisema suala hilo limepoteza amani ambapo wenzao wa vijiji viwili vya Wasa yenye wakazi 4800, Malolo wakazi 2700 na Isalalo wapo wakazi 2600 na Izyaniche wapo wakazi 1000 na kuwa madai yanayotolewa na wenzao wa vijiji hivyo ni ya kibinafsi zaidi ambayo wanaona yanawatenga licha ya kuwa wote ni jamii moja.

Kwa upande wake  Diwani wa kata hiyo ambaye pia anatokea kijiji cha Isalalo  Ezekiel Mwashambwa akizungumzia sakata hilo alisema  sababu za kuhamisha makao makuu ya kata ni kutokana na kuwa baadhi ya vijiji vilikuwa mbali na ofisi za kata ndipo walipopendekeza kwa halmashauri ya wilaya kuhamisha ofisi za kata ili ziwe katikati ya vijiji vyote vinne, ndipo kamati ya madiwani ya uchumi na mazingira ilipofika kujiridhisha na kupendekeza kwenye baraza kamili la madiwani ambalo lilidhia kuhamishwa ofisi hizo.

Alisema uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya kata ulipokelewa kwa mtazamo hasi na wakazi wa vijiji vingine viwili vya Wasa na Malolo hali iliyosababisha kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi wilaya Mbozi kufika katani hapo ndipo ilikutana na mabango yaliyodai kuwa kata haihamishiki na kutaka kumpiga diwani huyo hali iliyosababisha kukimbizwa na gari la chama lenye namba za usajili T. 595 BEW na  kisha kikao hicho kuvurugika.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mbozi  Elisey Ngoi akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi jana  alikiri kuwapo na mgogoro wa kugombea makao makuu ya kata katika kata hiyo na kudai kuwa suala hilo linafanyiwa kazi kwa kutumia busara  kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Songwe.

“ tumeona suala hili tulitatue kwa kutumia busara zaidi badala ya  kulichukulia kama ugomvi na njia nyingine kwani tunaona zitaharibu zaidi na kuendelea kuhatarisha amani katika maeneo hayo”alisema Ngoi.

Hata hivyo alikanusha kuwa wanafunzi  84 wa shule ya sekondari Isalalo waliohamia Msia ni kutokana na mtafaruku uliopo, bali alisema ni kutokana na kuwa Msia sekondari ipo jirani zaidi na makazi ya watoto hao ukilinganisha na Isalalo na kuwa katika kuthibitisha hili wazazi wa watoto hao kwa hiari yao walishiriki kukamilisha vyumba vya madarasa kwa nguvu yao ili watoto waanze kusoma.
Mwisho




 

No comments:

Post a Comment