Stephano Simbeye, MBOZI
Mlowo: Wakazi wa kitongoji cha Mtakuja
katika mji wa Mlowo wilayani Mbozi mkoani Songwe, wameridhia makazi yao
kupangwa upya ili kuwekwa miundombinu ya barabara na huduma nyingine za kijamii
pasipo kulipwa fidia, ili makazi yao yathaminishwe na kupatiwa hati miliki ya
ardhi huku wakitahadharisha wanasiasa kutoingilia zoezi hilo.
Makubaliano hayo yalifikiwa jana wakati wa mkutano wa uhamasishaji kabla
ya zoezi la kuanza kurasimisha na kupanga makazi yaliyojengwa kiholela, mpango
unaofanywa na Mpango wa kurasimisha rasilimali na biashara Tanzania (MKURABITA)
kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Mbozi ambapo wakazi wa eneo hilo
walilidhia licha ya kuitupia lawama serikali kufumbia macho wakati ujenzi
holela ukiendelea.
Jeradi Mwashilindi mkazi wa eneo hilo
alisema wanahamu kubwa ya kuona makazi yao yanaboreka na kuongezeka thamani
kuliko ilivyo sasa ambapo makazi yao yanakataliwa na wageni wanaohitaji kupanga
kutokana na maeneo hayo kukosa barabara
na kufanya yasifikike kirahisi.
"Mimi nilihamia hapa mwaka 1968
nikagawiwa kiwanja mwaka 1970 ambapo maeneo haya yalipimwa lakini yameendelea
kuvamiwa taratibu huku mamlaka husika zikifumbia macho"alisema mzee Mwashilindi
Mkazi mwingine wa kitongoji hicho Mariam
Mwinuka alitahadharisha zoezi hilo lisiingiliwe na wanasiasa kwa kuwa
watawagawa watu kwa itikadi zao hali ambayo itazua migogoro itakayokwamisha
mpango wa kurasimisha makazi yao.
Awali akihamasisha wananchi Ofisa mipango
miji wa halmashauri ya Mbozi Vitus Mwanalinze alieleza hatua tatu kuelekea
urasimishaji kuwa wameanza na hamasa, itafuatia kutambua makazi ambapo kila
mmiliki atapaswa kuwepo ili kutoa taarifa sahihi baada ya hapo itaandaliwa michoro
ya ramani (Deed plan) na kufuatiwa na urasimishaji wenyewe kazi hiyo itatumia
muda wa siku 20.
Alisema katika kutekeleza kazi hizo
hapatakuwa na fidia kwa makazi yatakayohitajika kubomolewa, bali wakazi wa
kitongoji husika watakubaliana jinsi ya kufanya ili kufanikisha zoezi.
Mwanalinze alisema mji wa Mlowo mpaka sasa
upimaji wa kawaida ulifanyika kwa asilimia 15 ambayo haiendani na kasi ya kukua
kwake na kwamba halmashauri imekwama kupima eneo lililobaki kutokana na
changamoto za kibajeti.
Naye ofisa Mtendaji wa kijiji cha Mlowo
Judith Mtega alisema kijiji hicho chenye wakazi 21181 kwa mujibu wa sensa ya
2012, lakini kinakabiliwa na ongezeko
kubwa la watu na makazi unaotokana na watu kuingia ili kufanya biashara na kuwa
chanzo cha ujenzi holela .
Meneja wa mpango wa kurasimisha rasilimali
na biashara Tanzania (MKURABITA) Japhet Werema alisema katika
kufanikisha kazi hiyo serikali metowa mtaji wa Sh. 17milioni ili kuanzia kazi
hiyo ya kupima na kurasimisha ardhi ya wanyonge na kuwa wananchi kwa upande wao
watachangia kidogo gharama hizo.
Alisema katika kutekeleza mpango huo wananchi walidhie wao
wenyewe kuachia baadhi ya maeneo ambamo
barabara zitapita na huduma nyingine za kijamii ziweze kuwafikia kirahisi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment