MOMBA: Kiwanda cha Chumvi kilichopo katika kijiji cha
Itumbula wilayani Momba mkoani Songwe kilichositisha uzalishaji miaka ya 80,
kinatarajia kuanza uzalishaji mapema mwezi Julai mwaka huu, baada ya kufanyiwa
ukarabati na halmashauri ya wilaya hiyo kufikia zaidi ya asilimia 90 na hivyo
zaidi ya watu 3000 kuanza kunufaika.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
Momba Adriano Jungu katika kikao cha Baraza kamili la Madiwani lililokutana mjini Chitete
kuwa, kazi ya kusafisha kisima kinachotoa madini joto imekamilika na kuwa kazi
inayoendelea ni kujenga mifereji ya maji ya mvua ili yasiingie kisimani na
kuchafua chumvi na kufanya marekebisho mengine madogo madogo na kuwa zaidi ya
Sh. 10 milioni zimetengwa kwa kazi hiyo.
Alisema iwapo kiwanda hicho kitaanza uzalishaji wananchi
zaidi ya 3000 wakazi wa kijiji hicho wataanza kunufaika kwa kuongeza kipato pia
halmashauri ya kijiji itaongeza mapato na halmashauri kwa ujumla itaongeza
mapato yake ya ndani yatakayotokana na ushuru na mzunguko wa fedha utaongezeka
kwa wafanyabiashara na kwamba uzalishaji wa chumvi kwa siku itakuwa kilogramu
500 au nusu tani.
“ Kiwanda hicho kilifungwa miaka mingi iliyopita kufuatia
ubadhirifu wa viongozi wa ushirika waliokuwa wakisimamia, hata hivyo suala la
uongozi limerekebishwa na kuwa halmashauri itakuwa karibu zaidi ili kuhakikisha
changamoto hiyo haijitokezi tena” alisema Mkurugenzi Jungu
Akizungumzia suala hilo diwani wa kata ya Kapele Gaasto
Simpassa alishauri wataalamu wanaofanyakazi za ukarabati eneo hilo kushirikiana
na wenyeji ili wawasaidie kutoa baadhi ya ushauri ili kufanikisha kazi hiyo
haraka.
Alisema wanayomatumaini na hamu kubwa kiwanda hicho kianze
kazi ili waanze kunufaika na fursa zitakazoambatana na shughuli hiyo ikiwa ni
pamoja na kuongeza kipato kufuatia ongezeko la watu na shughuli nyingi za
kiuchumi na kijamiii.
Mkazi wa eneo hilo Yusta Sichela alisema mradi huo utaleta
mabadiliko makubwa kijijini hapo kufuatia wageni wengi kwenda kununua chumvi na
hivyo wamejiandaa kuanza kutumia fursa hiyo kuboresha masha yao kwa kuinua
uchumi utakaotokana na huduma mbalimbali zitakazohitajika.
Alisema kiwanda hicho kilifungwa miaka ya 1980, changamoto
zilizosababisha kiwanda kufungwa zitazamwe vizuri ili tatizo hilo lisijetokea
tena na pia ameiomba serikali kuratibu kwa karibu shughuli za kiwanda hicho
ambacho ni fursa ya kuongeza kipato kwa wakazi wa kijiji na wilaya kwa ujumla
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Methew Chikoti aliwataka
wataalamu kuhakikisha wanasimamia kazi zilizosalia ili kukamilisha na
uzalishaji wa chumvi uanze katika muda uliopangwa na kuwa wanatarajia kikao
kijacho cha baraza la madiwani watapata taarifa ya kiwanda kuwa kimeanza kazi
na si vinginevyo
Mwisho.
No comments:
Post a Comment