Social Icons

Wednesday, 3 May 2017

RC; GALAWA AWAASA WAFANYAKAZI KUWA NA MALENGO YANAYOPIMIKA



Stephano Simbeye, ILEJE

Wafanyakazi mkoani Songwe, wametakiwa kwa kwa malengo ambayo yataleta tija inayoonekana kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuinua pato la mtu kutoka pato la sasa la Sh. 1.3 milioni na kuwa zaidi ya Sh. 7 milioni za lengo la Taifa kwa mwaka.

Mkuu wa mkoa wa Songwe Chiku Galawa alisema hayo jana wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani iliyoadhimishwa kimkoa mjini Itumba wilayani Ileje, kuwa kila mfanyakazi ni lazima awe na mpangokazi ambao utasaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa walengwa badala ya kutoa taarifa za maneno ambazo hazisaidii kuinua maisha ya watu.

Alitolea mfano kwa wataalamu wa ugani kuwa wanaweza kuweka lengo la kumwezesha mkulima kuongeza uzalishaji,mfano zao la mahindi kuwa hivi sasa wakulima wanapata gunia kati ya 8 na 15 kwa hekari moja hivyo anahitajika kuwezeshwa ili aongeze uzalishaji hadi kufikia gunia 25 na 30 kwa hekari moja hali kadhalika katika sekta nyingine zote zinapaswa kuwa hivyo.

“ acheni mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea timizeni wajibu wenu kwanza, mkifanikiwa kuongeza pato ndipo mdai haki maana iwapo mtaongeza pato la mwajiri ni rahisi kwake kuwaongeza stahiki zenu” alisema Galawa.

Awali katika risala ya wafanyakazi iliyisomwa na katibu wa CWT mkoa wa Songwe Emelia Mwakyoma alisema wafanyakazi wamekuwa wakifanyakazi kwa manung’uniko mengi yahusuyo upatikanaji wa stahiki zao ikiwemo kutolipwa madeni muda mrefu pamoja na kufanyika kwa zoezi la uhakiki.

Aidha Mwakyoma aliongeza kuwa suala la kuongezwa kwa makato ya wanufaika wa bodi ya mikopo ya elimu ya juu toka asilimia 8 hadi 15, imewaongezea wakati mgumu wa maisha watumishi kutokana na kuwa wengi wao wanakabiliwa pia na makato yanayotokana na mikpo waliyokopa toka taasisi za fedha na hivyo kufanya wasipate kitu chochote.

Mmoja wa wafanyakazi Edina Kalinga alisema wafanyakazi wapo tayari kufanya kazi kwa bidii na kwa malengo ya hali ya juu, lakini wamekuwa wakitatizwa na ukosefu wa vitendea kazi kama usafiri na rasilimali fedha ili kuweza kufika waliko wananchi na badala yake wanalaimika muda mwingi kuutumia wakiwa ofisini wakifanya kazi kwa kuagiza badala ya kufika wao wenyewe.

Alisema tunaiomba serikali iweke mazingira rahisi ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi kama usafiri ili kuwarahisishia kutimiza majukumu yao, pia iongeze bajeti ya uendeshaji.
Mwisho 

No comments:

Post a Comment