Social Icons

Tuesday, 19 December 2017

Halmashauri Songwe Zajikosesha Mamilioni ya Shilingi





Stephano Simbeye,

MBOZI: Halmashauri tano za mkoa wa Songwe zimeshindwa kuchangamkia fursa ya kupata zaidi ya Sh. 800milioni zinazotokana na malipo  kwa watoa huduma za afya yanyotolewa na mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) kufuatia kushindwa kuwasajili wazee zaidi ya 40000 ambao wangewezesha kupata fedha zaidi  kwa ajili ya kuboresha huduma ya afya kupitia mpango wa tele kwa tele. 

Kitendo hicho kimemkasilisha mkuu wa mkoa wa Songwe Chiku Galawa  ambapo alisema kitendo cha   kutotekeleza agizo lake la kuwalipia watu wenye umri wa zaidi ya miaka 60 badala ya kuwatengenezea vitambulisho vya msamaha vinavyogharimu Sh 5000 kila kimoja na badala yake wawalipie gharama ya kujiunga kwenye mfuko wa afya ya jamii (CHF) Sh. 10,000 fedha ambayo ingerejeshwa kwao mara mbili zaidi na mfuko wa taifa wa bima ya afya hivyo kuboresha upatikanaji wa dawa na vitendanishi.

 Naona suala la kuwalipia wazee ni mgomo kwa kuwa tuliagizana tangu mwaka jana lakini mlisingizia kuwa hamkuliweka katika bajeti,  mwaka huu mumeliweka kwenye bajeti lakini utekelezaji wake unasua sua tatizo lenu ni ubinafsi ingetokea safari hapa leo leo fedha zingepatikana mnajiangalia ninyi zaidi kuliko wengine kwa vile ninyi mkiugua mnapata matibabu” alisema Galawa.

“Mkiwalipia wazee mtarudishiwa fedha zenu kupitia mfuko wa tele kwa tele marambili na hivyo kuwa chanzo kingine cha mapato ambacho kitawasaidia kuboresha huduma za afya sijui ni kwanini hamtaki sasa nawaagiza na hapa sitaki mchezo ifikapo januari wazee wote muwe mumewaingiza kwenye mfuko wa bima ya afya ya jamii CHF na Bado mtatakiwa kuwalipia watoto na yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.  “ alisisitiza mkuu huyo wa mkoa.

Mkuu huyo wa mkoa alizungumza hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika mjini Vwawa katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi.

Wakijibu hoja ya mkuu wa mkoa wakurugenzi  wa halmashauri hizo walidai kwamba katika kipindi kilichopita walikuwa wakifanya kazi ya kuwatambua wazee kwanza ndipo hatua nyingine za kuwasajili katika mfuko wa afya ya jamii ifuate.

Kaimu Mkurugenzi mtendaji  katika halmashauri ya Mji wa Tunduma Kastroy Msigala alisema tayari halmashauri yake imewatambua wazee 1154 hatua za kuwalipia zimeanza isipokuwa bado  wazee 151 na kwamba wataongeza zaidi ili kukamilisha ifikapo Januari.

Mkurugenzi halmashauri ya Momba Adriano Jungu alikiri kuwa kulikuwa na matatizo ya Takwimu ambapo hadi sasa inaonesha kuna wazee 8000 katika halmashauri yake na kuwa michango iliyotolewea Januari Juni walililpia zaidi ya watu 50. 

Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani hapa alisema vituo vya afya vya serikali havichangamkii fursa iliwewekwa na serikali ambapo watoa huduma ya afya wanaowasajili wapata huduma za afya kupitia mfuko wa bima ya afya ya jamii wanapatiwa fedha nyingine kiasi kama hicho kwa lengo la kuboresha huduma za afya.

Alisema maelekezo ya fedha zinazorejeshwa kwa watumia huduma yanataka asilimia 77 ya fedha zinazorejeshwa zitumike kwa ajili ya kununua dawa na vitandanishi na kiasi kinachobaki kinaweza kutumika kwa matumizi mengine ya uendeshaji na kwamba halmashauri kutochangamkia hilo ni kupoteza fursa.

Aidha hadi sasa zaidi ya wazee  40402 wamekwishatambuliwa katika halmashauri zote mkoani hapa ambapo kila mmoja akilipiwa bima ya afya ya jamii kiasi cha Sh. 10,000 zitapatikana zaidi ya Sh. 404,020,000 ambazo zikitolewa mara dufu yake zinapatikana zaidi ya Sh. 808,040,000 ambazo zingesaidia kuboresha huduma za afya.
Mwisho





No comments:

Post a Comment