Social Icons

Wednesday, 20 December 2017

Wakulima Wataka Kupatiwa Mafunzo Kabla ya Msimu wa Kilimo Kuanza



Stephano Simbeye,  

MBOZI: Wakulima wa kikundi cha wakulima Ichenjezya Saccos wilayani Mbozi mkoani Songwe, wameomba kupatiwa mafunzo kwanza, kabla ya kuanza kulima na kupanda katika mashamba yao ili ujuzi wanaopata wautumie kwa vitendo mashambani mwao.

Hayo yamesemwa leo katika kijiji cha Nselewa ambako wakulima hao walikutana kwa ajili ya mafunzo katika shamba darasa ambapo walisema licha ya kupatiwa mafunzo hayo lakini tayari sehemu kubwa wamekwishalima na kupanda kwa mbinu walizozizowea jambo ambalo halijawasaidia sana.

Sekelo Kayange alisema kuanzia mwakani ni vizuri wakulima wa kikundi hicho wakapatiwa mafunzo kwanza katika shamba darasa, kabla ya kupatiwa pembejeo ndipo waendelee kuendeleza mashamba yao ili wataalamu wanapotoa mafunzo ya namna ya kupanda kwa kutumia pembejeo za kisasa ili katika muda ule ule waweze kutumia maarifa hayo kwenye mashamba yao ili kuleta tija.

“ wakulima wengi hawajachukulia suala la mafunzo kwa umuhimu unaopaswa, hivyo wanapaswa 
kujifunza kwanza ndipo hatua nyingine zifuate” alisema Kayange.

Katibu wa kikundi cha Ichenjezya Joseph  Masanja alisema wazo la kupatiwa mafunzo mapema waliliona lakini walipowasiliana na watu wa makampuni ya Mbegu walidai wasubiri mvua ziongezeke kwani kuanza kupanda katika mashamba darasa wakati mvua ni chache zinaweza zisiote vizuri kutokana na ukame lakini wakulima wakaona kama mbegu zao hazifai hazifai.

 “ hii ni changamoto kubwa maana kumfundisha mtu jinsi ya kupanda wakati alikwishap
anda haina maana yoyote lakini na sisi tumeliona jambo hilo tutalifanyia kazi ili mwakani yawepo marekebisho yatakayowasaidia wakulima ikibidi hata kumwagilia”alisema Masanja

Mtaalamu wa ugani aliyefika kuwafundisha wakulima hao Bornwelo Nzunda alisema wakulima wanatakiwa kuzingatia mafunzo yanayotolewa kupitia vikundi vyao kwa njia ya mashamba darasa kwani ni muhimu kufikisha maarifa yaliyokusudiwa kwao yatakayowasaidia kuboresha kilimo na kuwafanya waongeze tija.

Alieleza kusikitishwa na mahudhurio mabovu ya wakulima kwenye mafunzo jambo ambalo alisema litawafanya waendelee kurudi nyuma kiuzalishaji kwani kwa sasa ardhi inazidi kupungua huku watu wakiongezeka, kinachohitajika hapo ni kulima kilimo cha kisasa ambacho kitasaidia kupata mazao mengi katika eneo dogo.

Wiki iliyopita Mkuu wa mkoa Songwe Chiku Galawa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake aliagiza wataalamu wa ugani kuondoka ofisini na kuanzisha mashamba darasa katika maeneo yao ili wakulima wayatumie kupata maarifa yatakayowasaidia kuboresha kilimo chao ili kuongeza tija na kwamba hicho kitakuwa kipimo cha kila mgani.

Aidha Galawa alisema mkoa umeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji ikiwa ni pamoja na kudhibiti uingizaji wa pembejeo feki kwa kuwatambua wasambazaji wa pembejeo kila eneo ambapo alisema mkoa unatarajia kuongeza eneo la uzalishaji la hekta 299393 katika msimu wa kilimo 2017/2018 badala ya hekta 250117 zilizolimwa mwaka jana.
Mwisho. 




No comments:

Post a Comment