Stephano Simbeye,Mbozi
Wakulima wa mazao ya nafaka wilayani Mbozi mkoani Songwe
wametoa kilio chao cha kukabiliwa na changamoto ya kupangiwa bei ya mazao yao
pamoja na vipimo vya madebe na lumbesa ambavyo wanadai vinawanyonya, na kuitaka
Bodi ya mazao ya Nafaka na mazao mchanganyiko kuingia kazini ili kuwatetea.
Hayo yalisemwa jana kwa nyakati tofauti na wakulima wa
kijiji cha Ibembwa na wadau wa kilimo
wilayani hapa kuwa wameona huduma mbalimbali zikiwa na bei elekezi
ambayo huzingatia gharama za uzalishaji ili kumlinda mlengwa na kumpatia faida
kidogo ya kumwezesha kuzalisha zaidi.
Amasha Mwashiuya mkazi wa Ibembwa alisema wameona Bodi
nyingine za mazao mchanganyiko zikisimama imara kuwatetea wakulima wake, pia
wauzaji wa bidhaa nyingine ndio wanaopanga bei ya bidhaa zao lakini wakulima wa
mazao ya chakula wamekuwa wakipangiwa bei ya kuuza mazao yao na wanunuzi, huku
vikitumika vipimo visivyo halali jambo ambalo haliwezi kuwaondoa katika hali
duni.
“ Tunasikia kuna Bodi ya mazao mchanganyiko tunaiomba iingie
kazini itimize wajibu wake wa kututetea ili kuifanya kazi ya kilimo kuwa kazi
kama kazi nyingine, mbona tunaona huduma nyingine zinawekewa bei elekezi
imekuwaje kwa mazao ya nafaka ? “
aliuliza Amasha
David Mgogo alisema gharama ya kuzalisha mahindi kwa hekari
moja ni Sh. 372000 ambayo kwa wastani inampatia mkulima magunia 15 lakini
mahindi hayo yakiuzwa kwa bei iliyopo sasa sokoni ya Sh. 5000 kwa debe anapata
si zaidi ya Sh. 425000 jambo ambalo kwa hesabu ya kawaida haiwezi kumletea tija
mkulima kulinganisha na kazi anayofanya kwa msimu mzima.
Ekaristo Mgale alisema Bodi ya mazao ya nafaka na mazao
mchanganyiko ihakikishe inasimamia mazao kwa kuweka bei elekezi ili kudhibiti
masoko ili mkulima asiendelee kunyonywa, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku
upimaji mazao kwa kutumia madebe na lumbesa bali vitumike vipimo
vinavyotambulika kisheria.
“ tumekuwa tukisikia bei elekezi kwenye pembejeo, mafuta,
pamba, korosho, nauli za mabasi lakini kwenye mahindi yetu kwanini hatujawekewa
utaratibu huo tunaendelea kunyonywa lini nasi tutakomboka” alisema Mgale.
Afisa Kilimo wilayani hapa Richard Sirili akiongea na wadau
wa kilimo mwishoni mwa wiki alisema bei elekezi kwa mazao ya chakula, mazingira
mazuri ya soko vitasaidia kuhamasisha wakulima kuzalisha zaidi kwa kuwa hakuna
mtu anayeweza kuzalisha zaidi wakati hana uhakika na soko.
Aliwaonya wakulima kwa upande wao kuzingatia kanuni bora za
uzalishaji kwa kuzalisha mazo bora yenye
kiwango cha kimataifa ili nao waweze kuuza katika masoko ya nje pasipokuwa na
shida na kuacha kuchanganya mahindi mazuri na uchafu mwingine.
Kaimu Mkurugenzi wa shirika la MIICO Glory Mdindile alisema
kilimo nchini hakina mvuto hasa kwa vijana na wasomi kwa sababu hakilipi na
kuwa sababu kubwa ya wakulima kuendelea kuwa duni pamoja na jitihada kubwa ya
serikali kutaka kumuinua.
Kwa upande wake Katibu Tawala wilayani hapa Tusubilege
Benjamin alisema katika kuelekea uchumi wa kati wa viwanda mazao ya kilimo
ndiyo yanayotegemewa kuzalisha malighafi ya kulisha viwanda hivyo zinahitajika
jitihada mahususi ili kuboresha kilimo.
Aidha bei ya mazao ya chakula hususan mahindi imekuwa
ikiyumba ambapo mwaka jana mahindi yaliuzwa kati ya Sh. 800 kwa kilo, lakini
mwaka huu 2017 mahindi yanauzwa kati ya Sh. 200 kwa kilo wakati maharage
yanauzwa Sh. 1500 kwa kilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment