Social Icons

Monday, 1 January 2018

Wakulima Wataka Mazao yao Yapangiwe Bei elekezi



Stephano Simbeye,Mbozi

Wakulima wa mazao ya nafaka wilayani Mbozi mkoani Songwe wametoa kilio chao cha kukabiliwa na changamoto ya kupangiwa bei ya mazao yao pamoja na vipimo vya madebe na lumbesa ambavyo wanadai vinawanyonya, na kuitaka Bodi ya mazao ya Nafaka na mazao mchanganyiko kuingia kazini ili kuwatetea.

Hayo yalisemwa jana kwa nyakati tofauti na wakulima wa kijiji cha Ibembwa na wadau wa kilimo  wilayani hapa kuwa wameona huduma mbalimbali zikiwa na bei elekezi ambayo huzingatia gharama za uzalishaji ili kumlinda mlengwa na kumpatia faida kidogo ya kumwezesha kuzalisha zaidi.

Amasha Mwashiuya mkazi wa Ibembwa alisema wameona Bodi nyingine za mazao mchanganyiko zikisimama imara kuwatetea wakulima wake, pia wauzaji wa bidhaa nyingine ndio wanaopanga bei ya bidhaa zao lakini wakulima wa mazao ya chakula wamekuwa wakipangiwa bei ya kuuza mazao yao na wanunuzi, huku vikitumika vipimo visivyo halali jambo ambalo haliwezi kuwaondoa katika hali duni.

“ Tunasikia kuna Bodi ya mazao mchanganyiko tunaiomba iingie kazini itimize wajibu wake wa kututetea ili kuifanya kazi ya kilimo kuwa kazi kama kazi nyingine, mbona tunaona huduma nyingine zinawekewa bei elekezi imekuwaje kwa mazao ya nafaka ?  “ aliuliza  Amasha

David Mgogo alisema gharama ya kuzalisha mahindi kwa hekari moja ni Sh. 372000 ambayo kwa wastani inampatia mkulima magunia 15 lakini mahindi hayo yakiuzwa kwa bei iliyopo sasa sokoni ya Sh. 5000 kwa debe anapata si zaidi ya Sh. 425000 jambo ambalo kwa hesabu ya kawaida haiwezi kumletea tija mkulima kulinganisha na kazi anayofanya kwa msimu mzima.

Ekaristo Mgale alisema Bodi ya mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko ihakikishe inasimamia mazao kwa kuweka bei elekezi ili kudhibiti masoko ili mkulima asiendelee kunyonywa, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku upimaji mazao kwa kutumia madebe na lumbesa bali vitumike vipimo vinavyotambulika kisheria.

“ tumekuwa tukisikia bei elekezi kwenye pembejeo, mafuta, pamba, korosho, nauli za mabasi lakini kwenye mahindi yetu kwanini hatujawekewa utaratibu huo tunaendelea kunyonywa lini nasi tutakomboka” alisema Mgale.

Afisa Kilimo wilayani hapa Richard Sirili akiongea na wadau wa kilimo mwishoni mwa wiki alisema bei elekezi kwa mazao ya chakula, mazingira mazuri ya soko vitasaidia kuhamasisha wakulima kuzalisha zaidi kwa kuwa hakuna mtu anayeweza kuzalisha zaidi wakati hana uhakika na soko.

Aliwaonya wakulima kwa upande wao kuzingatia kanuni bora za uzalishaji kwa kuzalisha mazo bora  yenye kiwango cha kimataifa ili nao waweze kuuza katika masoko ya nje pasipokuwa na shida na kuacha kuchanganya mahindi mazuri na uchafu mwingine.

Kaimu Mkurugenzi wa shirika la MIICO Glory Mdindile alisema kilimo nchini hakina mvuto hasa kwa vijana na wasomi kwa sababu hakilipi na kuwa sababu kubwa ya wakulima kuendelea kuwa duni pamoja na jitihada kubwa ya serikali kutaka kumuinua.

Kwa upande wake Katibu Tawala wilayani hapa Tusubilege Benjamin alisema katika kuelekea uchumi wa kati wa viwanda mazao ya kilimo ndiyo yanayotegemewa kuzalisha malighafi ya kulisha viwanda hivyo zinahitajika jitihada mahususi ili kuboresha kilimo.

Aidha bei ya mazao ya chakula hususan mahindi imekuwa ikiyumba ambapo mwaka jana mahindi yaliuzwa kati ya Sh. 800 kwa kilo, lakini mwaka huu 2017 mahindi yanauzwa kati ya Sh. 200 kwa kilo wakati maharage yanauzwa Sh. 1500 kwa kilo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment