Stephano Simbeye, MBOZI:
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Hamidu
Aweso amewataka wataalamu wa maji nchini kushirikisha wananchi katika kutafuta
vyanzo vya maji na katika kutambua maeneo halisi yenye uhaba wa maji wakati wa
kusambaza.
Kauli hiyo aliitoa jana katika kijiji cha Itaka kufuatia
malalamiko ya mkazi wa kijiji cha Itewe Sikujua Mwankusye kuwa yameachwa maeneo
halisi yenye uhaba wa maji badala yake yamepelekwa katika maeneo yasiyo na
uhaba mkubwa na kuwaacha wananchi wakiendelea kutabika kupata maji huku wakiona
wenzao wakineemeka wakati tayari wanapata huduma hiyo jirani na visima vya
asili.
“ Mheshimiwa Naibu Waziri tunashangaa wataalamu kuweka vituo
vya maji katika maeneo ambayo tayari kuna maji huku wakiacha kwenye mapungufu
makubwa bila kituo chochote cha maji: alisema Mwankusye.
Mwenyekiti wa kijiji cha Itewe Efeso John alipoitwa kuelezea
namna vituo vilivyopatikana alisema wataalamu wa maji walifika kijijini hapo na
kasha kuanza kuonyesha maeneo yatakayowekwa vituo vya kuchotea maji na kwamba
hawakushirikishwa ili kutambulisha kwenye uhaba wa maji.
Alisema baada ya kuona eneo moja ndani ya kijiji chao lenye
uhitaji mkubwa wa maji halijawekwa kwenye mpango wa kupatiwa maji licha ya
mradi kuwepo kijijini hapo walihoji lakini walijibiwa kwamba hawawezi kuyavusha
maji barabara.
Mhandisi wa maji wilayani hapa Crispin Warioba alikanusha
madai hayo na kueleza kwamba hatua zote serikali za vijiji na umoja wa watumia
maji zilishirikishwa katika kutambua maeneo yote ambayo yaliwekwa kwenye mpango
wa kuwekwa vituo vya kuchotea maji na kuwa madai yanayotolewa si ya kweli.
Alisema hata hivyo iwapo kuna mapungufu yaliyojitokeza
yanaweza kurekebishwa kwa kuwa mradi upo hatua za mwanzo ambapo umefikia
asilimia 10 tangu uanze kujengwa.
Warioba alibainisha kwamba mradi una thamani ya zaidi ya Sh.
1.67 bilioni unatarajia kuhudumia vijiji vine vya Itewe, Itaka, Hangomba na
Bara na kuwa umeanza kujengwa tanki
lenye ujazo wa lita 150000 na unatarajia kuwanufaisha wakazi 32935 umeanza mwezi Novemba mwaka huu na utakamilika Juni
mwaka ujao.
Aidha naibu waziri Aweso alisema serikali ya awamu ya tano
chini ya kampeni yake ya kumtua mama ndoo kichwani inawataka wataalamu na
viongozi kutokuwa kikwazo cha kufanikisha kampeni hiyo badala yake watoke
maofisini na kuhangaika kufanikisha azma hiyo.
Alisema wakati wa kutafuta vyanzo vya maji washirikishe
wakazi wa maeneo husika kupitia mikutano ya hadhara ili kubaini uhaba halisi wa
maji ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.
Awali Mbunge wa Jimbo la Mbozi Pascal Haonga alisema jimbo
lake linakabiliwa na kero kubwa ya maji ambayo inasababisha ndoa kuvunjika na
migogoro hivyo kuiomba serikali kutatua kero hiyo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment