Social Icons

Thursday, 8 February 2018

CCM Yapiga Marufuku Kutangaza nia kabla ya Muda kwenye maeneo yanayoongozwa na viongozi wake



Stephano Simbeye, MBOZI: 

Chama cha Mapinduzi mkoani Songwe kimepiga marufuku wanachama wake wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho katika maeneo yanayoongozwa na viongozi wenye dhamana ya chama hicho kwa lengo la kushawishi wapiga kura ili waje kuwachagua katika uchaguzi ujao kuwa watachukuliwa hatua kari.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa chama hicho mkoani hapa Mercy Moleli jana Februari 4, mwaka huu katika kilele cha maadhimisho ya miaka 41 ya CCM yaliyofanyika kimkoa katika kata ya Mlangali wilayani Mbozi kuwa kanuni za chama hicho haziruhusu mwanachama kwenda kupita katika eneo analoongoza kiongozi anayetokana na chama hicho ikiwa bado muda wake wa kutekeleza ilani unaendelea.

“msiwasumbue Viongozi wenye dhamana ya CCM waliopo madarakani waacheni waendelee kutekeleza Ilani ya uchaguzi msije mkawakosesha usingizi badala ya kuwaza kuwatumikia wananchi waanze kuwaza masuala ya uchaguzi nyuma” alisema Moleli na kuongeza kuwa.

“ Tunataka viongozi wetu washughulike na shida za wananchi wetu, washughulike na upungufu wa vyumba vya madarasa, washughulike na ukosefu wa pembejeo, washughulikie kero ya maji na kero za miundombinu vijijini” alisema katibu huyo wa CCM mkoani hapa.

Mkazi mmoja wa kijiji cha Ndolezi kata ya Mlangali Amenye Mwasibha alisema wapo watu ambao wameanza kupita huku na kule wakitumia matatizo ya wananchi kuwarubuni kwa kuwapatia vizawadi ili waje kuwachagua katika uchaguzi ujao.

Alisema watu hao wanawachonganisha na viongozi waliopo madarakani licha ya kufanya kazi zao vizuri lakini wanawavuruga na hivyo kuwachanganya.

Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) Stanslaus Nsojo akizungumza katika mkutano huo aliwataka watendaji wa serikali kutoa majibu haraka kwa wananchi wanapowasilisha kero zao na kuzifanyia kazi haraka na zinazowashinda kuziwasilisha kwa wahusika.

Alisema hatamvumilia kiongozi yeyote ambaye atashindwa kushirikiana na CCM katika kutatua kero zinazowakabili wananchi kwa kisingizio chochote.

Aidha katika maadhimisho hayo CCM imevuna wanachama 1004 kutoka vyama vya Chadema na CUF ambao wamerejesha kadi za vyama vyao na kujiunga na chama hicho katika kipindi cha wiki moja ya maadhimisho ya kutimiza miaka 41 tangu kuanzishwa kwake.
Mwisho.

1 comment: