Stephano Simbeye, MBOZI:
Chama cha Mapinduzi mkoani Songwe kimepiga marufuku
wanachama wake wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama
hicho katika maeneo yanayoongozwa na viongozi wenye dhamana ya chama hicho kwa
lengo la kushawishi wapiga kura ili waje kuwachagua katika uchaguzi ujao kuwa
watachukuliwa hatua kari.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa chama hicho mkoani hapa
Mercy Moleli jana Februari 4, mwaka huu katika kilele cha maadhimisho ya miaka 41
ya CCM yaliyofanyika kimkoa katika kata ya Mlangali wilayani Mbozi kuwa kanuni
za chama hicho haziruhusu mwanachama kwenda kupita katika eneo analoongoza
kiongozi anayetokana na chama hicho ikiwa bado muda wake wa kutekeleza ilani
unaendelea.
“msiwasumbue Viongozi wenye dhamana ya CCM waliopo
madarakani waacheni waendelee kutekeleza Ilani ya uchaguzi msije mkawakosesha
usingizi badala ya kuwaza kuwatumikia wananchi waanze kuwaza masuala ya
uchaguzi nyuma” alisema Moleli na kuongeza kuwa.
“ Tunataka viongozi wetu washughulike na shida za wananchi
wetu, washughulike na upungufu wa vyumba vya madarasa, washughulike na ukosefu
wa pembejeo, washughulikie kero ya maji na kero za miundombinu vijijini”
alisema katibu huyo wa CCM mkoani hapa.
Mkazi mmoja wa kijiji cha Ndolezi kata ya Mlangali Amenye
Mwasibha alisema wapo watu ambao wameanza kupita huku na kule wakitumia
matatizo ya wananchi kuwarubuni kwa kuwapatia vizawadi ili waje kuwachagua
katika uchaguzi ujao.
Alisema watu hao wanawachonganisha na viongozi waliopo
madarakani licha ya kufanya kazi zao vizuri lakini wanawavuruga na hivyo
kuwachanganya.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC)
Stanslaus Nsojo akizungumza katika mkutano huo aliwataka watendaji wa serikali
kutoa majibu haraka kwa wananchi wanapowasilisha kero zao na kuzifanyia kazi
haraka na zinazowashinda kuziwasilisha kwa wahusika.
Alisema hatamvumilia kiongozi yeyote ambaye atashindwa
kushirikiana na CCM katika kutatua kero zinazowakabili wananchi kwa kisingizio
chochote.
Aidha katika maadhimisho hayo CCM imevuna wanachama 1004
kutoka vyama vya Chadema na CUF ambao wamerejesha kadi za vyama vyao na
kujiunga na chama hicho katika kipindi cha wiki moja ya maadhimisho ya kutimiza
miaka 41 tangu kuanzishwa kwake.
Mwisho.
Thumb up!
ReplyDelete