Na: Mwandishi Wetu, Mbozi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Jenista Mhagama amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa zilizopo kwenye
maeneo yao kwa kuanzisha vijiwe vya kiuchumi.
Kauli hiyo ameitoa na Waziri
Mhagama wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo na miradi ya vijana
iliyopo katika Kituo cha Maendeleo ya Vijana, Sasanda kilichopo Kata ya
Nyimbili, Mkoani Songwe.
Akiwa katika ziara hiyo Mhe. Mhagama alieleza kuwa, Serikali ya
awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
imeendelea kutimiza azima yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, hivyo vijana
watumie fursa hiyo kujifunza mambo muhimu na kuanzisha viwanda vidogo vidogo
ambavyo vitawafanya wabadilishe vijiwe wanavyokaa kuwa vya kiuchumi.
“Tunataka kuona vijana watakapo jifunza kilimo bora, ufugaji wa ng’ombe au
nyuki wataweza kuboresha thamani mazao na bidhaa kwa kuanzisha viwanda vidogo
ndani ya Mkoa wa Songwe, mkakati
wetu katika kituo hiki ni kutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana
kuongeza thamani ya mazao na bidhaa watakazozalisha ambazo zitakuwa ni
kichocheo muhimu katika kufikia maendeleo yao” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa, Takribani
vijana 500 kwenye kituo hicho wamejifunza stadi za maisha, ufundi na elimu
mbalimbali zinazotolewa kwenye kituo ambazo zitawawezesha kujipatia kipato.
Sambamba na hilo, Mhe. Mhagama
aliwahimiza Viongozi wa Mkoa kushirikiana na Ofisi yake ili waweze kuwasaidia
vijana ambao wamekwisha anzisha viwanda vidogo vidogo ndani ya mkoa huo kwa kuwawezesha
kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuwatafutia soko la uhakika ndani na nje ya
nchi.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa
rai kwa vijana kujiunga kwenye vikundi ambavyo ni endelevu na vyenye muelekeo wa kuanzisha viwanda
vidogo vitakavyowawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao na pelekea
kufikia uchumi wa kati kama mpango wa maendeleo wa taifa unavyoelekeza.
Pia, aliwaelezea juu ya
uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo zitafanyika katika Mkoa huo na
kuwataka vijana na wanawake kutumia fursa hiyo kuutangaza vyema mkoa wa Songwe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi alieleza kuwa kituo cha Maendeleo ya
Vijana cha Sasanda kimewawezesha vijana kujitambua na kujiwekea malengo ya maisha
na kuyatekeleza kwa faida yao, jamii na taifa kwa ujumla.
“Tunatarajia kuanzisha mafunzo
na programu zitakazowaelekeza vijana masuala ya kilimo biashara ambacho
kitasaidia upatikanaji wa malighafi zitakazokuwa zinahitajika kwenye viwanda
vilivyopo nchini,” alisema Kajugusi
Naye Bw. Silia Kibona ambaye
ni mnufaika kupitia kituo hicho, aliishukuru Serikali kwa kuwajengea mazingira ya
kujifunzia ambayo yamewasaidia kupata mafunzo muhimu na aliwahamasisha vijana
wenzie kuhudhuria mafunzo yanayotolewa kwenye kituo hicho.
Kituo cha Maendeleo ya Vijana
– Sasanda kilianzishwa mwaka 1979 kwa ushirikiano wa Serikali kupitia Wizara ya
Utamaduni wa Taifa, Vijana na Michezo iliyopo wakati huo pamoja na Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Uanzishaji wa Kituo hicho ulifuatia kuanzishwa kwa
mpango wa kuunda vikundi vya vijana vya uzalishaji mali, uliolenga kuwawezesha
vijana wasio na ajira kuweza kujiunga na kufanya kazi za kujitegemea hasa
katika sekta ya kilimo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment