Mashabiki wa Soka katika mji wa Vwawa wilayani Mbozi
mkoani Songwe wamesema mashindano ya ligi ya Mabingwa wa mikoa kanda, yatawanufaisha kibiashara na kuwawezesha upya kuona mashindano
makubwa baada ya timu ya Kimondo SC kushuka daraja miaka mitatu iliyopita.
Mmoja wa mashabiki wa mchezo wa soka wilayani hapa David
Mwaibhofu alisema Songwe kupewa kituo cha mashindano hayo ni fursa kubwa ya
kufanya biashara kwa kuwa wachezaji na baadhi ya mashabiki wao watakuwa
wakipata huduma za kijamii zilizopo mkoani hapa hivyo kuongeza mzunguko wa
fedha.
Alisema faida nyingine watakayoipata ni pamoja na kupata
burudani ya mashindano makubwa waliyoikosa katika kipindi kirefu tangu kushuka
kwa timu za Kimondo Sc na Karume Ranfers.
“uwanja mzuri tunao lakini hatuoni mashindano makubwa, hii
ni changamoto kwa wadau wote wa michezo kushikamana ili kuwa na timu walau moja
itakayoshiriki mashindano makubwa ya kitaifa”alisema David.
Naye Obadia Chilale alisema mashabiki wamefurahia kuanza kwa
mashindano hayo kwani katika kipindi kirefu hawajapata burudani, lakini pia
alieleza changamoto kwa chama cha mpira wa miguu mkoani hapa kuyatangaza zaidi
ili wengi wafahamu na wapate nafasi ya kufika uwanjani kushuhudia timu
zikimenyana.
Mmoja wa wachezaji wa Timu ya DTB Fc Juma A. Juma alisema
mashindano hayo yatakuwa na ushindani mkubwa kutokana na kuwa kila timu iliyopo
imekuja kwa lengo la kushinda na kusonga mbele katika hatua inayofuata.
“ timu zote zicheze mpira uwanjani zisitegemee mteremko
maana kila mmoja amekuja kwa malengo yake ya kutaka kusonga mbele hakuna
aliyekuja kwa lengo la kushindwa” alisema Juma
Kwa upande wake msemaji wa timu ya Nzihi Fc Jirani Hassan
alisema licha ya timu yake kupoteza mchezo wa kwanza watajipanga vizuri ili
kuhakikisha wanashinda michezo inayofuata.
Mashindano ya ligi ya mabingwa wa mikoa yaliyoanza jana
katika vituo vinne hapa nchini na kukamilika April 11 mwaka huu ambapo timu 28
zinatarajia kumenyana vikari katika makundi hayo yatakayofanyika katika mikoa
ya Simiyu, Katavi, Songwe, na Dodoma ambapo kila kundi litatoa washindi wawili
ambao wataingia hatua ya nane bora ambayo washindi watatu wa juu watacheza ligi
daraja la pili Tanzania Bara.
Mwisho
No comments:
Post a Comment