Social Icons

Thursday, 28 March 2019

NMB Yatoa Msaada wa Sare za Vijana wa Halaiki Uzinduzi wa Mbio za Mwenge


Na: Mwandishi Wetu, Mbozi

Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemus Mwangela leo amepokea msaada wa Sare za vijana wa Halaiki katika sherehe za uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 na madawati 120 kwa ajili ya shule mbili za sekondari vyote vyenye thamani ya zaidi ya Sh.29.8Milioni kutoka Benki ya NMB.

Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Songwe Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Straton Chilongola alisema lengo la Benki yake ni kusaidia maendeleo ya jamii kupitia Nyanja za elimu na Afya na kwamba benki hiyo imetenga zaidi ya Sh.1bilioni kwa ajili hiyo.

Alifafanua kuwa benki hiyo imetoa Truck Suit 800 kwa ajili ya vijana wa halaiki ya Mwenge zenye thamani ya Sh.19,824,000 na msaada wa viti na meza 120 kwa ajili ya shule za sekondari za Ndugu na Vwawa Day zote zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Mbozi yenye thamani ya Sh.10milioni na kufanya msaada huo kuwa na thamani ya Sh.29,824,000.

Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo Mkuu huyo wa mkoa alisema NMB ni wadau muhimu wa maendeleo ya wananchi na kwamba imekuwa benki ya mfano kwa utoaji huduma bora kwa wajasiriamali, wakulima kupitia Amcos na hata kwa mtu mmoja mmjoa.

Alisema michango ya NMB katika kuleta maendeleo imejikita katika masuala ya msingi ya elimu na afya kwa kuwa wanatambua umuhimu wa elimu na afya katika jamii na kuwa suala la afya pia ni pamoja na masuala ya michezo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment