Na Mwandishi wetu
Timu ya Soka ya DTB FC toka Dar se salaam imeanza vizuri
kusaka tiketi ya kuwania kufuzu katika Ligi ya mabingwa wa mikoa katika kituo cha
Songwe, baada ya kuichapa timu ya Nzihi FC Wanyalukolo toka Iringa kwa jumla ya
mabao 2 – 1 katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa katika uwanja wa CCM Vwawa
wilayani Mbozi.
Mchezo huo ambao ulianza kwa kila timu kusoma mchezo wa
mwenzake ambapo katika dakika 45 za kipindi cha kwanza timu zote zilitoka suluhu bila kufungana.
DTB FC ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata Bao la kwanza katika
dakika 60 ya mchezo lililofungwa na
Dickson Samson, bao hilo lilidumu kwa muda wa dakika 17 baadaye kabla ya timu
ya Nzishi Fc ya Iringa kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Isaack Kivamba
katika dakika ya 75 ya mchezo.
Hata hivyo kupatikana kwa baola kusawazisha kuliamsha ari ya
wachezaji wa timu zote mbili kuanza kushambuliana kwa zamu na kuwa bahati
ilikuwa ya DTB FC ambao walipata bao katika dakika 3 za nyongeza, hivyo hadi mwamuzi wa mchezo huo Ahamad Kikumbo anapuliza kipenga cha kuashiria
kumalizika dakika 90 za mchezo timu ya DTB FC ilikuwa mbele kwa mabao 2 – 1.
Kwa upande wake Kocha wa timu ya Nzihi Fc Edger Nzelu
alisema vijana wake walicheza vizuri lakini kutokana na maamuzi mabovu ya
mwamuzi na utelezi uwanjani uliosababishwa na mvua, wamepoteza mchezo huo hata
hivyo alisema watajipanga vizuri katika machezo ujao ili kufanya vizuri zaidi.
Naye kocha wa timu ya DTB FC Kambi M. Kambi alisema timu
pinzani muda wote walikuwa wakicheza mchezo wa kuotea ambao wachezaji wake
walipoung’amua imesaidia kupata ushindi baada ya kutumia makosa ya wapinzani
wao.
Kituo cha Songwe kina jumla ya timu 7 za DTB Fc Dar es
salaam), Nzihi Fc (Iringa), Mpera Pesa (Songwe), makete United (Njombe), Top
Boys (Ruvuma), Coast Star (Pwani) na Dipotivo Mang’ula (Morogoro) na kwamba
mashindano hayo yanatarajia kuendelea kesho ambapo kutakuwa na michezo miwili
itakayohusisha timu 4.
Mchezo wa kwanza utakaoanza saa 8 mchana utakuwa ni kati ya
wenyeji Mpera Pesa na Dipotivo Mang’ula ya Morogoro na mchezo wa pili utakuwa
kati ya Makete United ya Njombe na Top Boys ya Ruvuma, michezo yote itachezwa
katika uwanja wa CCM Vwawa wilayani Mbozi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment