Na Jonas Simbeye, Tunduma
Waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa amekuja na matumaini
kwa wakazi wa mkoa wa Songwe hususani miji ya Vwawa, Itumba Isongole na Tunduma
ya kuwapatia maji safi na salama kufuatia Serikali kuwalipa madeni ya
Makandarasi waliyokuwa wakiidai, na hivyo kufanya miradi hiyo kukwama na sasa
itaendelea hadi kumalizika.
Alisema miradi mitatu mikubwa ya maji yenye thamani ya zaidi
ya Sh. 3.2 bilioni katika wilaya tatu za mkoa wa Songwe, iliyokuwa imekwama
kukamilika kwa sababu za ukosefu wa fedha inatarajia kukamilika mwezi mmoja toka sasa na kuanza kutoa maji.
Waziri Mbarawa
alisema hayo katika ziara yake ya
kukagua miradi hiyo ambayo imekwama kutokana na ukosefu wa fedha na kuwa sasa
Makandarasi hao wamelipwa fedha zao kilichobaki ni kuwasimamia wamalize kazi walizopewa ili wananchi waanze
kupata maji.
Alisema lengo la ziara yake ni kupita kwenye miradi yenye
changamoto kubwa ambazo zimekwamisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
kumtua mwanamke ndoo kichwani.
Mbarawa aliitaja baadhi ya miradi mkoani Songwe yenye
changamoto kuwa ni pamoja na mradi wa maji Vwawa, Itumba – Isongole, Tunduma na
mradi wa maji Tindingoma katika halmashauri ya wilaya ya Momba ambao alizuia
fedha ili ajiridhishe kwa kuutembelea ndipo fedha zitolewe.
Awali Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu
Nicodemas Mwangela akizungumza wakati wa kutoa taarifa yab hali ya maji mkoani
hapa ambayo ni asilimia 46.3 katika maeneo ya vijijini na aslimia 40.8 kwenye
maeneo ya mjini na kuwa na wastani wa jumla wa upatikanaji wa huduma ya maji
mkoani hapa kuwa asilimia 45.3.
Alisema pia mkoa unakabiliwa na changamoto ya Makandarasi
kutolipwa fedha zao kwa wakati hali inayofanya miradi ya maji kutokamilika kwa
wakati, ambapo miradi hiyo ilipaswa iwe imekamilika tangu Desemba 31 mwaka juzi
lakini kutokana na sababu hiyo ililazimika kuongeza muda.
Kwa upande wake Mhandisi wa maji Mamlaka ya maji na usafi wa
mazingira Mbeya Ndele Mengo alifafanua kuwa mradi wa maji Vwawa umefikia kiwango cha asilimia 90 ili
ukamilike, Itumba Isongole asilimia 84 na Tunduma asilimia 96 na kwamba miradi
hiyo imesalia kazi ndogondogo za umaliziaji.
Mkandarasi anayejenga mradi wa maji Itumba Isongole wilayani
Ileje toka kampuni ya Singirimu Enterprises Abdala Digelo alieleza sababu za
kushindwa kukamilika kwa mradi huo kuwa ni pamoja na kushindwa kufikisha vifaa
eneo la ujenzi kutokana na mvua kunyesha na baadhi ya vifaa kutopatikana kwa
wauzaji.
Naye Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Leo start
engeneering Johanes Mgosi inayojenga
mradi maji Vwawa Johanes Mgosi alieleza
sababu za kuchelewa kwa mradi huo kuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha na kuwa
alithibitisha mradi huo kukamilika baada ya wiki mbili toka sasa baada ya
kuwasili Pump aliyoiagiza na kisha kuanza kufanya kazi ya kufunga mita kwa
watumia maji.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo alisema wilaya
yake imeandika andiko la mradi mkubwa wa maji wa kutosha vijiji 12 ambao upo
Wizarani iwapo ukikamilika utasaidia kupunguza uhaba wa maji hadi kufikia
asilimia zaidi ya 90 hivyo kumuomba Waziri asaidie.
Mwisho
No comments:
Post a Comment