Social Icons

Monday, 19 March 2018

TFS Yashauriwa Kuweka Vivutio vya Utalii ndani ya Hifadhi ya Misitu yake



Stephano Simbeye,ILEJE:   
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kanda ya nyanda za juu kusini umeshauriwa kuanzisha maeneo ya vivutio vya watalii ndani ya hifadhi ili kuwezesha kuwepo utalii wa misitu kwa kuweka vituo vya kupumzikia  (Camping site) ili kukuza sekta ya utalii katika mikoa hiyo.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri Maliasili na Utalii Japheti Hasunga alipokagua msitu wa Iyondo Mswima wenye ukubwa wa hekta 12053 uliopo wilayani Ileje mkoani Songwe kuwa serikali imedhamilia kukuza sekta ya utalii na hasa katika ukanda wa kusini ambao sekta hii haikutiliwa mkazo miaka mingi ili kuongeza watalii wengi na pato la Taifa.

Alisema katika mikoa hiyo vipo  vivutio vingi vya utalii ambavyo pia havijabainishwa vinavyoweza kufanya utalii katika mikoa hiyo na kufanya wananchi wakapata ajira na wakapiga hatua katika maisha yao.

“ Nawashauri bainisheni vivutio vilivyopo ili viwekewe mkakati mahususi wa kuvitangaza na sambamba na hilo hamasisheni wafanyabiashara kujenga mahoteli mazuri ya kitalii pamoja na kumbi za mikutano ili watalii wakija wapate sehemu ya kulala, lakini pia wahamasisheni waanzishe makampuni ya kuongoza watalii ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto fani za kuongoza watalii” alisema Hasunga

Hasunga alisema kwa kuanzia katika eneo la hifadhi ya msitu wa serikali wa Iyondo Mswima na  mingine wakala wa huduma za misitu wabuni njia ya kufanya ili kuanzisha utalii wa misitu ambao unaweza ukawekewa vivutio vingine kama utamaduni wa asili ili kuwafanya watalii kuvutika na hivyo kukaa muda mrefu katika maeneo hayo na kuongeza kipato na ajira kwa wananchi.

Aidha aliongeza kuwa serikali imeanzisha mradi mkubwa wa kufufua utalii katika Ukanda wa Kusini na kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini kutoka watalii 1489 mwaka jana hadi kufikia watalii zaidi ya 2800 ifikapo 2020 na kuongeza pato litokanalo na utalii kutoka dola za kimarekani 2bilioni hadi dola za kimarekani 5bilioni.

Awali akiwasilisha taarifa Meneja wa Msitu wa Iyondo Mswima Ibrahimu Msinga msitu huo umetowa ajira kwa watu 400 katika msimu wa upandaji miti na kwamba mwaka huu unatarajia kuongeza ajira za watu 250 baada ya shughuli kuongezeka kwa ajili ya kuhudumia bustani ya miti na kazi ya upandaji.

Aidha alisema wakala huo umetowa miti 300 kwa halmashauri ya wilaya ya Ileje kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwa wananchi ili kuimarishja mahusiano mema baina ya wananchi na wakala huo(TFS) hata hivyo alisema ipo changamoto ya wananchi kuingilia eneo la misitu ambapo wamepanda miti yao binafsi katika eneo la zaidi ya hekta 40.5 kutokana na maeneo hayo kuwa wazi muda mrefu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ileje Ubatizo Songa alisema kutokana na kuanzishwa kwa hifadhi yam situ huo halmashauri yake itaangalia namna ya kupanua wigo ili kufanya wilaya inufaike na wananchi wake waweze kuongeza kipato kupitia misitu na utalii.

Alisema katika wilaya hiyo vipo vivutia vingi vya utalii ambavyo havijatangazwa kama wanyama aina ya Mbega ambao ni adimu hapa nchini lakini wanapatikana wilayani humo, maanguko ya mito ambayo pia yanaweza kuwa vivutio lakini kutokana na kutoitangazwa vivutio hivyo havijawanufaisha.

Mmoja wa wakazi wa kata ya Sange ulipo msitu huo Sailas Kibona alisema kutokana na hali ya hewa na mazingira ya eneo walilolopo ya safu nyingi za milima, anaamini linaweza kuwa kivutio kikubwa cha utalii hivyo kuwanufaisha kwa kupata ajira na kipato.

Alisema pia uwepo wa kisitu katika eneo lao umechangia kwa sehemu kubwa kuwapatia kipato kwani katika maeneo yao ardhi kwa ajili ya kilimo cha mazao ni kidogo hivyo wanatumia misitu kujiongezea kipato kwa kupasua mbao na kuziuza.

Kwa upande wake Katibu Tawala wilayani humu Mary Joseph alisema kitendo cha serikali kuu kupitia wakala wa hifadhi ya misitu Tanzania kuanzisha mradi katika wilaya hiyo utasaidia kuibadilisha wilaya ya Ileje kutoka hapo ilipo sasa na kuwa yenye uchumi mkubwa katika kipindi cha miaka 20 ijayo na kuwa wilaya yenye viwanda vin gi vya mbao na kukuza pato la wilaya.

Alimuomba Naibu Waziri Maliasili na Utalii kuangalia pia msitu wa asili wa Kyosa uliopo wilayani humo ambao kwa hivi sasa unakabiliwa na uharibifu mkubwa ili kuona namna ambavyo serikali kupitia wakala wa huduma za misitu ili kuuhifadhi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Aidha katika mkoa wa Songwe vipo vivutio vingi ikiwemo Kimondo cha Mbozi, mapango ya popo, chemichemi za maji moto, unyayo wa binadamu katika jiwe, matanuru ya kale na vingine vingi ambavyo iwapo vitawekewa mkazo vinaweza kusaidia kuinua utalii katika ukanda huu.
Mwisho.


3 comments:

  1. habari, samahan naomba mawasiliano ya uongozi wa shamba la miti la iyondo mswima lililotembelewa na makamu wa rais.

    nahitaj kutuma maombi ya kazi.

    nahitaj email au namba ya mfanyakazi yeyote wa hapo

    ReplyDelete
  2. Mbona hamjaweka mawasiliano kama mtu anataka kufika hasa kuona maji moto au vivutio hivyo? Naomba mawasiliano

    ReplyDelete