Social Icons

Featured Posts

Sunday, 31 March 2019

Waziri Mbarawa Awajia Juu Halmashauri ya Momba

Na: Jonasi Simbeye, Chitete


Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza chanzo cha mgogoro uliyopo  katika mradi wa maji Chitete katika wilayani Momba mkoani Songwe, ambapo halmashauri imevunja mkataba na kumweka mkandarasi mwingine kinyume cha taratibu  na kuchelewesha mradi.

Alisema mradi wa maji Chitete wenye thamani ya Sh.493.2milioni  Umekuwa na mabishano ambayo yanasababisha mradi kuchelewa kukamilika na hivyo kuwafanya wananchi waendelee kukosa huduma ya maji iliyokusudiwa.

“ DC upo hapa naagiza Takukuru waje wafanye uchunguzi wabaini nini kimejificha katika mzozo huo, kama kuna interest za watu tujue na wakati huo tuiombe wakala wa manunuzi (PPRA) watoe ufafanuzi juu ya suala kama hili ili kuondoa ubishani na ili mradi uendelee” alisema Mbarawa

Alisema chanzo cha mabishano hayo ni kufuatia Mkandarasi wa kwanza kuchelewa kufika eneo la kazi ambapo halmashauri ilichukua hatua ya kuvunja mkataba, na kumuweka mkandarasi mwingine   jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu kwa kuwa halmashauri baada ya kuvunja mkataba ilipaswa ipate kibari toka Wizarani kisha taratibu nyingine za manunuzi zingefuata.

Mhandisi wa Maji wilaya ya Momba Maua Mgala alisema chanzo cha mgogoro huo ni mkandarasi kutoonekana eneo la kazi katika kipindi cha miezi mitano tangu alipokabidhiwa kazi, jambo ambalo ni kinyume cha mkataba ambao unaeleza kuwa mkandarasi asipoonekana kwenye eneo la kazi mkataba utavunjwa.

“mkandarasi huyu alisaini mkataba Julai 12 mwaka 2017 lakini hakuonekana hadi Februari 26 mwaka 2018 ambapo ndipo mkataba ulipovunjwa nay eye kujulishwa ndipo alipoleta vifaa vichache na kuandika barua ya kupinga kuvunjwa kwa mkataba”alisema Mgala

Alifafanua kuwa hata hivyo alisema halmashauri ilimvumilia mkandarasi huyo huku ikimwandikia barua za kumkumbusha lakini hakutokea ndipo ilipovunja mkataba na kumchukua mkandarasi aliyeshika nafasi ya pili kwenye zabuni ili aendelee na kazi hiyo.

Kuhusu uamuzi wa Waziri kufuatia sakata hilo Mhandisi Maua alisema ni uamuzi mzuri ambao utatupeleka mahali pazuri na hatimaye kukamilisha mradi ili wananchi waendelee kupata maji.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Momba Adriano Jungu alimwambia Waziri wa Maji kwamba lilipojitokeza suala la utata wa Mkandarasi huyo alikwenda moja kwa moja Wizarani ili kutoa maelezo ya jinsi hatua mbalimbali alizozichukua kuhusu mkandarasi huyo.

Aidha Kampuni ya DIPE & Company Limited ya Morogoro ndiyo iliyoshinda kandarasi ya kujenga mradi wa maji Chitete wenye thamani ya zaidi ya Sh.493.2 milioni, ambapo wakati wa ziara ya Waziri Mbarawa hakuna mwakilishi wa kampuni hiyo aliyekuwepo.

Friday, 29 March 2019

Habari katika Picha Ziara ya Waziri wa Maji mkoani Songwe

 Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa mwenye kofia kulia akiangalia mtambo wa kusafishia maji katika mradi wa maji Vwawa (Mantengu) alipotembelea jana ili kukagua maendeleo yake akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani Songwe.
 Waziri Mbarawa akikagua ujenzi wa tanki la kusafishia maji katika mradi wa maji Vwawa
 Katibu wa CCM mkoa wa Songwe Bi. Mercy Moleli akitoa neno la shukrani kwa Serikali ya awamu ya tano kwa Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa, hapo ni juu ya tanki la maji katika mradi wa maji Itumba Isongole, kulia kwake ni Mkuu wa wilaya ya Ileje Joseph Mkude
 Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa akipokelewa na baadhi ya viongozi katika halmashauri ya Mji wa Tunduma alipowasili kukagua miradi ya maji.
 Tanki la maji katika mradi wa maji wa Itumba - Isongole
Kisima cha maji ambacho kitatumika kusambaza maji katika mradi wa maji Tunduma ambao ni moja ya miradi iliyotembelewa jana na Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa.

Waziri Mbarawa Awapa Matumaini Mapya ya Kupata Maji Wananchi


Na  Jonas Simbeye, Tunduma

Waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa amekuja na matumaini kwa wakazi wa mkoa wa Songwe hususani miji ya Vwawa, Itumba Isongole na Tunduma ya kuwapatia maji safi na salama kufuatia Serikali kuwalipa madeni ya Makandarasi waliyokuwa wakiidai, na hivyo kufanya miradi hiyo kukwama na sasa itaendelea hadi kumalizika.

Alisema miradi mitatu mikubwa ya maji yenye thamani ya zaidi ya Sh. 3.2 bilioni katika wilaya tatu za mkoa wa Songwe, iliyokuwa imekwama kukamilika kwa sababu za ukosefu wa fedha inatarajia kukamilika  mwezi mmoja toka sasa na kuanza kutoa maji.

 Waziri Mbarawa alisema hayo  katika ziara yake ya kukagua miradi hiyo ambayo imekwama kutokana na ukosefu wa fedha na kuwa sasa Makandarasi hao wamelipwa fedha zao kilichobaki ni kuwasimamia  wamalize kazi walizopewa ili wananchi waanze kupata maji.

Alisema lengo la ziara yake ni kupita kwenye miradi yenye changamoto kubwa ambazo zimekwamisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya kumtua mwanamke ndoo kichwani.
Mbarawa aliitaja baadhi ya miradi mkoani Songwe yenye changamoto kuwa ni pamoja na mradi wa maji Vwawa, Itumba – Isongole, Tunduma na mradi wa maji Tindingoma katika halmashauri ya wilaya ya Momba ambao alizuia fedha ili ajiridhishe kwa kuutembelea ndipo fedha zitolewe.

Awali Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemas Mwangela akizungumza wakati wa kutoa taarifa yab hali ya maji mkoani hapa ambayo ni asilimia 46.3 katika maeneo ya vijijini na aslimia 40.8 kwenye maeneo ya mjini na kuwa na wastani wa jumla wa upatikanaji wa huduma ya maji mkoani hapa kuwa asilimia 45.3.

Alisema pia mkoa unakabiliwa na changamoto ya Makandarasi kutolipwa fedha zao kwa wakati hali inayofanya miradi ya maji kutokamilika kwa wakati, ambapo miradi hiyo ilipaswa iwe imekamilika tangu Desemba 31 mwaka juzi lakini kutokana na sababu hiyo ililazimika kuongeza muda.

Kwa upande wake Mhandisi wa maji Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Mbeya Ndele Mengo alifafanua kuwa mradi wa maji Vwawa  umefikia kiwango cha asilimia 90 ili ukamilike, Itumba Isongole asilimia 84 na Tunduma asilimia 96 na kwamba miradi hiyo imesalia kazi ndogondogo za umaliziaji. 

Mkandarasi anayejenga mradi wa maji Itumba Isongole wilayani Ileje toka kampuni ya Singirimu Enterprises Abdala Digelo alieleza sababu za kushindwa kukamilika kwa mradi huo kuwa ni pamoja na kushindwa kufikisha vifaa eneo la ujenzi kutokana na mvua kunyesha na baadhi ya vifaa kutopatikana kwa wauzaji.

Naye Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Leo start engeneering  Johanes Mgosi inayojenga mradi maji Vwawa  Johanes Mgosi alieleza sababu za kuchelewa kwa mradi huo kuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha na kuwa alithibitisha mradi huo kukamilika baada ya wiki mbili toka sasa baada ya kuwasili Pump aliyoiagiza na kisha kuanza kufanya kazi ya kufunga mita kwa watumia maji.

Naye Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo alisema wilaya yake imeandika andiko la mradi mkubwa wa maji wa kutosha vijiji 12 ambao upo Wizarani iwapo ukikamilika utasaidia kupunguza uhaba wa maji hadi kufikia asilimia zaidi ya 90 hivyo kumuomba Waziri asaidie.
Mwisho


Thursday, 28 March 2019


Katika picha ni Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemus Mwangela (wa kwanza toka kushoro mwenye miwani na shati la kitenge), kulia kwake ni Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Benki ya NMB Straton Chilongola na wa mwisho kulia kwa Meneja wa NMB ni Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo, wakwanza kulia kwa RC ni Katibu wa CCM mkoa wa Songwe Bi. Mercy Moleli.

NMB Yatoa Msaada wa Sare za Vijana wa Halaiki Uzinduzi wa Mbio za Mwenge


Na: Mwandishi Wetu, Mbozi

Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemus Mwangela leo amepokea msaada wa Sare za vijana wa Halaiki katika sherehe za uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 na madawati 120 kwa ajili ya shule mbili za sekondari vyote vyenye thamani ya zaidi ya Sh.29.8Milioni kutoka Benki ya NMB.

Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Songwe Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Straton Chilongola alisema lengo la Benki yake ni kusaidia maendeleo ya jamii kupitia Nyanja za elimu na Afya na kwamba benki hiyo imetenga zaidi ya Sh.1bilioni kwa ajili hiyo.

Alifafanua kuwa benki hiyo imetoa Truck Suit 800 kwa ajili ya vijana wa halaiki ya Mwenge zenye thamani ya Sh.19,824,000 na msaada wa viti na meza 120 kwa ajili ya shule za sekondari za Ndugu na Vwawa Day zote zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Mbozi yenye thamani ya Sh.10milioni na kufanya msaada huo kuwa na thamani ya Sh.29,824,000.

Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo Mkuu huyo wa mkoa alisema NMB ni wadau muhimu wa maendeleo ya wananchi na kwamba imekuwa benki ya mfano kwa utoaji huduma bora kwa wajasiriamali, wakulima kupitia Amcos na hata kwa mtu mmoja mmjoa.

Alisema michango ya NMB katika kuleta maendeleo imejikita katika masuala ya msingi ya elimu na afya kwa kuwa wanatambua umuhimu wa elimu na afya katika jamii na kuwa suala la afya pia ni pamoja na masuala ya michezo.
Mwisho

Wednesday, 27 March 2019

“Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kituo cha Songwe Yapokelewa kwa Shangwe na Mashabiki”



Na Mwandishi Wetu, Mbozi

Mashabiki wa Soka katika mji wa Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe wamesema  mashindano ya ligi ya Mabingwa wa mikoa kanda, yatawanufaisha kibiashara na kuwawezesha upya kuona mashindano makubwa baada ya timu ya Kimondo SC kushuka daraja miaka mitatu iliyopita.

Mmoja wa mashabiki wa mchezo wa soka wilayani hapa David Mwaibhofu alisema Songwe kupewa kituo cha mashindano hayo ni fursa kubwa ya kufanya biashara kwa kuwa wachezaji na baadhi ya mashabiki wao watakuwa wakipata huduma za kijamii zilizopo mkoani hapa hivyo kuongeza mzunguko wa fedha.

Alisema faida nyingine watakayoipata ni pamoja na kupata burudani ya mashindano makubwa waliyoikosa katika kipindi kirefu tangu kushuka kwa timu za Kimondo Sc na Karume Ranfers.
“uwanja mzuri tunao lakini hatuoni mashindano makubwa, hii ni changamoto kwa wadau wote wa michezo kushikamana ili kuwa na timu walau moja itakayoshiriki mashindano makubwa ya kitaifa”alisema David.

Naye Obadia Chilale alisema mashabiki wamefurahia kuanza kwa mashindano hayo kwani katika kipindi kirefu hawajapata burudani, lakini pia alieleza changamoto kwa chama cha mpira wa miguu mkoani hapa kuyatangaza zaidi ili wengi wafahamu na wapate nafasi ya kufika uwanjani kushuhudia timu zikimenyana.

Mmoja wa wachezaji wa Timu ya DTB Fc Juma A. Juma alisema mashindano hayo yatakuwa na ushindani mkubwa kutokana na kuwa kila timu iliyopo imekuja kwa lengo la kushinda na kusonga mbele katika hatua inayofuata.

“ timu zote zicheze mpira uwanjani zisitegemee mteremko maana kila mmoja amekuja kwa malengo yake ya kutaka kusonga mbele hakuna aliyekuja kwa lengo la kushindwa” alisema Juma

Kwa upande wake msemaji wa timu ya Nzihi Fc Jirani Hassan alisema licha ya timu yake kupoteza mchezo wa kwanza watajipanga vizuri ili kuhakikisha wanashinda michezo inayofuata.

Mashindano ya ligi ya mabingwa wa mikoa yaliyoanza jana katika vituo vinne hapa nchini na kukamilika April 11 mwaka huu ambapo timu 28 zinatarajia kumenyana vikari katika makundi hayo yatakayofanyika katika mikoa ya Simiyu, Katavi, Songwe, na Dodoma ambapo kila kundi litatoa washindi wawili ambao wataingia hatua ya nane bora ambayo washindi watatu wa juu watacheza ligi daraja  la pili Tanzania Bara.

Mwisho

Ligi ya Mabingwa wa Mikoa Yaanza Kituo cha Songwe


Na Mwandishi wetu

Timu ya Soka ya DTB FC toka Dar se salaam imeanza vizuri kusaka tiketi ya kuwania kufuzu katika  Ligi ya mabingwa wa mikoa katika kituo cha Songwe, baada ya kuichapa timu ya Nzihi FC Wanyalukolo toka Iringa kwa jumla ya mabao 2 – 1 katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa katika uwanja wa CCM Vwawa wilayani Mbozi.

Mchezo huo ambao ulianza kwa kila timu kusoma mchezo wa mwenzake ambapo katika dakika 45 za kipindi cha kwanza  timu zote zilitoka suluhu bila kufungana.

DTB FC ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata Bao la kwanza katika dakika 60 ya mchezo  lililofungwa na Dickson Samson, bao hilo lilidumu kwa muda wa dakika 17 baadaye kabla ya timu ya Nzishi Fc ya Iringa kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Isaack Kivamba katika dakika ya 75 ya mchezo.

Hata hivyo kupatikana kwa baola kusawazisha kuliamsha ari ya wachezaji wa timu zote mbili kuanza kushambuliana kwa zamu na kuwa bahati ilikuwa ya DTB FC ambao walipata bao katika dakika 3  za nyongeza, hivyo hadi mwamuzi wa mchezo huo  Ahamad Kikumbo anapuliza kipenga cha kuashiria kumalizika dakika 90 za mchezo timu ya DTB FC ilikuwa mbele kwa mabao 2 – 1.

Kwa upande wake Kocha wa timu ya Nzihi Fc Edger Nzelu alisema vijana wake walicheza vizuri lakini kutokana na maamuzi mabovu ya mwamuzi na utelezi uwanjani uliosababishwa na mvua, wamepoteza mchezo huo hata hivyo alisema watajipanga vizuri katika machezo ujao ili kufanya vizuri zaidi.

Naye kocha wa timu ya DTB FC Kambi M. Kambi alisema timu pinzani muda wote walikuwa wakicheza mchezo wa kuotea ambao wachezaji wake walipoung’amua imesaidia kupata ushindi baada ya kutumia makosa ya wapinzani wao.

Kituo cha Songwe kina jumla ya timu 7 za DTB Fc Dar es salaam), Nzihi Fc (Iringa), Mpera Pesa (Songwe), makete United (Njombe), Top Boys (Ruvuma), Coast Star (Pwani) na Dipotivo Mang’ula (Morogoro) na kwamba mashindano hayo yanatarajia kuendelea kesho ambapo kutakuwa na michezo miwili itakayohusisha timu 4.

Mchezo wa kwanza utakaoanza saa 8 mchana utakuwa ni kati ya wenyeji Mpera Pesa na Dipotivo Mang’ula ya Morogoro na mchezo wa pili utakuwa kati ya Makete United ya Njombe na Top Boys ya Ruvuma, michezo yote itachezwa katika uwanja wa CCM Vwawa wilayani Mbozi.
Mwisho.